Matthew 12:1-8

Bwana Wa Sabato

(Marko 2:23-28; Luka 6:1-5)

1 aWakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. 2 bLakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”

3 cYesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? 4 dAliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. 5 eAu hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? 6 fNawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. 7 gKama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, 8 hkwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Copyright information for SwhNEN